TIMU ya Taifa ya Kilimanjaro Stars kesho jioni itashuka kwa mara ya pili kwenye dimba la uwanja wa taifa wa Addis Ababa Ethiopia kukabiliana na Rwanda ‘Amavubi.

Mechi hiyo inatarajia kuwa ya ushindani mkubwa  kutokana na Tanzania na Rwanda kuwa timu zenye ushindani mkubwa katika soka ya ukanda wa Mashariki na Kati na wachezaji wake kujuana vizuri.


Timu zote mbili zinaingia uwanjani kesho zikiwa zimetoka kupata ushindi Rwanda wakiwafunga wenyeji Ethiopia kwa bao 1-0, katika mchezo wa ufunguzi wakati Kili Stars iliifunga Somalia mabao 4-0 na kuifanya iongoze kundi A, kutokana na idadi kubwa ya mabao.

Kujuana kwa wachezaji wa timu zote mbili na kucheza soka la kufanana ndiko kunakoufanya mchezo huo kuwa mgumu na siyo rahisi kutabiri timu gani inaweza kuibuka na ushindi.


Mara ya mwisho timu hizo kukutana ilikuwa uwanja wa taifa Dar es Salaam, katika michuano hiyo ya mwaka 2012, Rwanda ikifundishwa na kocha Milutin Micho ambaye kwa sasa anaifundisha Uganda iliifunga Kili Stars mabao 3-1.

Kila timu inaingia uwanjani ikiwa imeshinda mechi yake ya kwanza jambo linalozidi kufanya ugumu katika mechi hiyo na kuwa isiyotabirika.


Kili Stars ilifanya ‘mauaji’ katika mechi ya kwanza baada ya kuishushia kipondo cha mabao 4-0 Somalia mwishoni mwa wiki iliyopita huku Rwanda ikiwafunga wenyeji Ethiopia bao 1-0 katika mechi ya ufunguzi.

Pengine mchezo wa kesho ukawa ni wakulipiza kisasi kwa Kili Stars, kutokana na uimara iliyokuwa nao hivi sasa chini ya kocha Abdallah Kibaden, lakini hata kikosi cha Rwanda siyo cha kubeza hasa baada ya kuwafunga wenyeji kwenye mchezo wa ufunguzi.


Ushindi kwa kila timu katika mechi hiyo ni muhimu ili kuendelea kuongoza kundi hilo na kuweka matumaini ya kucheza hatua ya robo fainali.

Kwa mujibu wa kanuni za michuano hiyo timu mbili za juu kutoka kila kundi kati ya makundi matatu zitafuzu robo fainali pamoja na timu mbili zilizoshika nafasi ya tatu kwa uwiano mzuri ‘best loser’ na kufanya idadi ya timu nane zitakazocheza robo fainali.


Katika kundi A mpaka sasa Kili Stars na Amavubi zipo kwenye nafasi nzuri baada ya kushinda mechi zao za kwanza.

Nahodha wa Kili Stars John Bocco  aliyefunga mabao mawili katika mchezo dhidi ya Somalia amesema  hana shaka na kupata matokeo mazuri kwenye mchezo wa kesho kwasababu wachezaji wote wana ari kubwa kuhakikisha wanabeba ubingwa wa kombe hilo mwaka huu.


Amesema baada ya mechi dhidi ya Somalia timu yake imeimarika zaidi na morali yao iko juu kutaka ushindi.

“Morali yetu iko juu kwa sasa tumeshasahau matokeo mabaya yaliyopita na sasa tunataka kushinda kwenye kombe la Chalenji… baada ya mechi na Somalia timu yetu ipo vizuri sana,” amesema.



Rwanda inaongwa za nahodha Haruna Niyonzima ambaye katika mchezo wa kwanza alianzia benchi nao wana matumaini ya kuendeleza rekodi yao ya kuifunga Kili kwenye fainali hizo.

Niyonzima anayetarajiwa kuanza kwenye mchezo wa kesho anauhakika wa kupata ushindi kutokana na kuwajua vizuri wachezaji wa Tanzania hivyo haoni kikwazo cha kuwazuia wasiweze kufanya vizuri.

Mchezo huo utapigwa kuanzia majira ya saa10 jioni na mpaka sasa hakuna utabiri unaoonyesha kuupa ushindi upande wowote kutokana na timu hizo kuonyesha kiwango kinachofanana kwenye mchezo wa kwanza.